TRUMP AMUONYA KAIMU RAIS WA VENEZUELA KUWA ANAWEZA KULIPA GHARAMA KUBWA KULIKO YA MADURO
Rais wa Marekani Donald Trump anasema Makamu wa Rais wa Venezuela Delcy Rodriguez anaweza kulipa gharama kubwa zaidi kuliko kiongozi aliyeondolewa madarakani Nicolas Maduro "ikiwa hatafanya yaliyo sawa", kulingana na mahojiano na jarida la The Atlantic.
"Ikiwa [Delcy Rodriguez] hatafanya yaliyo sawa, atalipa gharama kubwa sana, labda kubwa kuliko Maduro," alisema Trump.
Kiongozi huyo wa Marekani alikuwa akijibu kile alichokielezea kama kukataa kwa Rodriguez kuingilia kati kwa Marekani kwa silaha kulikosababisha kukamatwa kwa Maduro.
Awali Trump alimsifu Rodriguez siku ya Jumamosi baada ya vikosi vya Marekani kumkamata Maduro na mkewe. Hata hivyo, Rodriguez alisema baadaye kwamba nchi yake italinda maliasili zake.
Rais wa Marekani alitetea uamuzi wake wa kumchukua Maduro kwa nguvu, akiambia jarida hilo: "Unajua, kujenga upya huko na mabadiliko ya utawala, chochote unachotaka kukiita, ni bora kuliko kile ulicho nacho sasa. Haiwezi kuwa mbaya zaidi."
Trump pia alisema nchi zingine zinaweza kuingiliwa na Marekani. "Tunahitaji Greenland, bila shaka," alisema kuhusu kisiwa hicho ambacho ni sehemu ya Denmark, nchi ya NATO.
