TULGWU YAIPONGEZA SERIKALI YA AWAMU YA SITA
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
CHAMA cha Watumishi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TULGWU) kimeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi zake za kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma, huku kikieleza matumaini mapya katika kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta ya utumishi wa serikali za mitaa.
Pongezi hizo zimetolewa jijini Dodoma wakati wa Kikao cha 31 cha Baraza la Taifa la TULGWU, ambapo Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Deus Sangu, amesema kuwa mkutano huo ni haki ya kikatiba na ni sehemu ya misingi ya demokrasia na ushirikishwaji wa watumishi wa umma katika maamuzi yanayowahusu.
Amesema watumishi wa serikali za mitaa ni mhimili muhimu katika utoaji wa huduma kwa wananchi, akibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha mazingira ya kazi ikiwemo upandishwaji wa madaraja, ajira mpya hususan katika sekta ya afya, pamoja na kuimarisha vyama vya wafanyakazi.
“Licha ya kipindi kigumu ambacho ajira zilisimama, Rais alitoa ajira na anaendelea kufanya hivyo Serikali inaendelea kuthamini mchango wa watumishi wa umma,” amesema Waziri huyo.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wa serikali za mitaa ili kuongeza ufanisi, na kuwataka watumishi kuzingatia maadili ya utumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi.
Kuhusu changamoto ya fedha za likizo, Waziri amesema kuwa suala hilo limekuwa kero kwa muda mrefu, lakini tayari mapendekezo yalishawasilishwa na Serikali inaendelea kushughulikia malimbikizo ya madai hayo ili watumishi walipwe stahiki zao.
Aidha, ameuelezea uboreshaji wa miundo ya utumishi kwa baadhi ya kada kuwa ni hatua muhimu itakayowezesha watumishi wanaoongeza elimu kunufaika kitaaluma, tofauti na hali ya awali iliyokuwa ikiwakatisha tamaa.
Akisoma risala ya TUGWU, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Komredi Wandiba Ngocho, amesema chama kinaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kusikiliza na kushughulikia kero za watumishi wa umma, hususan katika maeneo ya upandishwaji wa madaraja, uboreshaji wa maslahi, ujenzi wa vituo vya afya, mafunzo kazini pamoja na maboresho ya mifumo ya rasilimali watu.
Hata hivyo, Komredi Ngocho ameeleza kuwa bado kuna changamoto ya kutolipwa kwa wakati fedha za likizo kwa watumishi wa serikali za mitaa, akibainisha kuwa baadhi yao hawajalipwa tangu mwaka 2018.
Amesema chama kinaomba serikali itenge fedha maalum ili kumaliza tatizo hilo ambalo linaendelea kuongezeka kila mwaka.
Ametaja kero nyingine kuwa ni pamoja na kutolipwa kwa wakati fedha za uhamisho, pamoja na vitendo vya kuwadhalilisha watumishi wa umma wanapotekeleza majukumu yao, hususan katika sekta ya afya.
Amehimiza viongozi wa kisiasa kufuata taratibu za kisheria na kuheshimu haki na hadhi ya watumishi wa umma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUGWU Taifa, Tumaini Yamuhoka, amesema chama hicho kimeendelea kuwa mshirika mwaminifu wa Serikali, kikizingatia misingi ya mazungumzo na ushirikiano badala ya migomo.
“Sisi ni watumishi wa umma wanaoheshimu utaratibu TUGWU si chama cha migomo, bali tunaamini katika majadiliano, na kwa kiasi kikubwa mambo yanaendelea vizuri,” amesema Yamuhoka.
Kikao hicho kimeelezwa kuwa ni fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na watumishi wa serikali za mitaa kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kulinda maslahi ya watumishi.











