HONGERA SANA GANGILONGA PRE AND PRIMARY SCHOOL NI USHAHIDI TOSHA UBORA WA SHULE ZA SERIKALI
Kwa muda mrefu, kumekuwepo na mtazamo hasi kutoka kwa baadhi ya watu dhidi ya shule za serikali, ambapo zimekuwa zikibeza na kuziita kwa majina yasiyofaa kama vile “St Kayumba”, wakimaanisha kuwa ni shule zisizo na ubora wa elimu.
Hata hivyo, matokeo ya hivi karibuni ya Gangilonga Pre and Primary School yameibua mjadala mpana na muhimu katika jamii, kwa wananzi wa darasa la Nne kufanya vizuri na kupata darasa A na B pekee tofauti na shule binafsi ambazo baadhi zina hadi D,matokeo haha yakionesha wazi kuwa shule za serikali zina uwezo mkubwa wa kutoa elimu bora yenye viwango vya juu vya taaluma kama zilivyo shule nyingine zote, ikiwemo zile za binafsi.
Matokeo haya mazuri si ya bahati mbaya. Ni matokeo ya juhudi za pamoja na ushirikiano imara kati ya uongozi wa shule, walimu, wazazi, wanafunzi pamoja na mmiliki wa shule ambaye ni Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Kwa msingi huo, pongezi za dhati zinastahili kutolewa kwa uongozi wa Manispaa ya Iringa kwa kusimamia vyema shule hii, kuhakikisha mazingira rafiki ya kujifunzia, pamoja na kuweka mikakati ya kuinua taaluma kwa vitendo.
Walimu wa Gangilonga Pre and Primary School wameonesha mfano wa kuigwa kwa kujituma, kujali wanafunzi, na kutambua wajibu wao mkubwa katika kujenga kizazi chenye maarifa, maadili na uzalendo.
Pamoja na changamoto mbalimbali zinazokabili shule nyingi za serikali, walimu hawa wameendelea kufanya kazi kwa moyo, wakitumia rasilimali zilizopo kwa ubunifu na weledi mkubwa.
Hili linadhihirisha kuwa ubora wa elimu haupimwi kwa majengo makubwa au ada kubwa, bali kwa dhamira ya walimu na mfumo mzima wa usimamizi wa elimu.
Vilevile, mchango wa wafanyakazi wasio walimu haupaswi kusahaulika nidhamu, usafi, na usalama wa mazingira ya shule ni matokeo ya kazi yao ya kila siku.
Mazingira salama na yenye utulivu humwezesha mwanafunzi kujifunza kwa kujiamini na kuzingatia masomo yake kikamilifu.
Hii ni sehemu muhimu ya mafanikio ambayo mara nyingi haitajwi sana, lakini ina mchango mkubwa katika matokeo ya kitaaluma.
Wazazi nao wamekuwa nguzo muhimu ya mafanikio haya. Ushirikiano wao na uongozi wa shule, kuhudhuria vikao, kufuatilia maendeleo ya watoto wao na kutoa mchango wao pale inapohitajika, kumeongeza ufanisi wa malezi na elimu kwa ujumla.
Ushirikiano kati ya shule na wazazi ni silaha kubwa katika kuboresha elimu, na Gangilonga Pre and Primary School imeonesha kwa vitendo umuhimu wa mshikamano huo.
Mafanikio ya shule hii yanapaswa kuwa somo kwa jamii nzima juu ya umuhimu wa kuzikubali, kuzithamini na kuziamini shule zetu za serikali.
Shule za serikali ndizo zinazohudumia idadi kubwa ya watoto wa Kitanzania, na ndizo msingi wa usawa wa elimu kwa wote bila kujali hali ya kiuchumi.
Kuzibeza shule hizi ni sawa na kudhoofisha juhudi za taifa katika kujenga rasilimali watu bora kwa maendeleo ya nchi.
Ni muhimu kubadili mtazamo na kuwekeza imani katika shule za serikali pale jamii, serikali na wadau wa elimu wanaposhirikiana, matokeo chanya hujitokeza kama ilivyo kwa Gangilonga Pre and Primary School.
Badala ya kuzipa majina ya kejeli, tunapaswa kuzitambua kama shule zenye uwezo mkubwa, zinazohitaji kuungwa mkono, kuimarishwa na kupewa heshima stahiki.
Kwa ujumla, mafanikio ya Gangilonga Pre and Primary School ni ushahidi tosha kwamba shule za serikali zinaweza na zinafanya vizuri. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuzipigia debe, kuzilinda na kushiriki katika kuziboresha.
Zaina Mlawa mkurungenzi Manispaa ya IrongaHongera tena kwa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa chini ya mkurugenzi Zaina Mlawa, Mstahiki meya Ibrahim Ngwada ,uongozi wa shule, walimu, wafanyakazi na wazazi wote.
Meya Iringa Ibrahim NgwadaHii ni hatua muhimu kuelekea kubadili fikra za jamii na kujenga mustakabali bora wa elimu nchini Tanzania.


