Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
IRUWASA YAPATA CHETI CHA PONGEZI TOKA JESHI LA POLISI

IRUWASA YAPATA CHETI CHA PONGEZI TOKA JESHI LA POLISI


 Na Matukio Daima Media 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limetoa cheti cha shukrani kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Iringa (IRUWASA) kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuboresha huduma za maji kwa jeshi hilo pamoja na jamii kwa ujumla.

Hafla ya utoaji wa cheti hicho imefanyika usiku wa leo katika ukumbi wa Masiti, Gangilonga mjini Iringa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Familia ya Jeshi la Polisi maarufu kama Police Family Day Iringa 2026.

 Maadhimisho hayo yamelenga kuimarisha mshikamano, mahusiano mema na kutambua mchango wa wadau mbalimbali wanaoshirikiana na jeshi la polisi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Kheri James, ambaye amepongeza uongozi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kwa hatua ya kutambua na kuthamini mchango wa wadau wake.

 Mheshimiwa Kheri James amesema ushirikiano kati ya taasisi za umma ni jambo muhimu katika kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi na kusaidia jeshi la polisi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Ameongeza kuwa IRUWASA imekuwa mfano mzuri wa taasisi inayotekeleza wajibu wake kwa weledi na uwajibikaji, hususan katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa makazi ya askari polisi, vituo vya polisi na wananchi wa Manispaa ya Iringa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limesema IRUWASA imekuwa mshirika wa karibu kwa muda mrefu, hususan katika kuhakikisha huduma ya maji haikatiki katika maeneo nyeti ya kiusalama, jambo ambalo limechangia kuboresha mazingira ya kazi na maisha ya askari polisi na familia zao.

Mhandisi David Pallangyo mkurugenzi wa IRUWASA 

Cheti cha shukrani kwa IRUWASA kimepokelewa na Afisa Mahusiano wa mamlaka hiyo, Restituta Sakala, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa IRUWASA, Mhandisi David Pallangyo. 


Sakala alilishukuru jeshi la polisi Mkoa wa Iringa  na uongozi mzima wa jeshi hilo kwa kutambua mchango wa IRUWASA, na kuahidi kuwa mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na jeshi la polisi pamoja na wadau wengine katika kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira kwa maendeleo ya Mkoa wa Iringa.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3