KADA WA CHADEMA IRINGA AVUTIWA NA UJENZI WA BARABARA YA LAMI MKIMBIZI
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Iringa Mjini, Christopher Mbunda, amepongeza ujenzi wa barabara ya lami unaoendelea katika Kata ya Mkimbizi, Manispaa ya Iringa, akisema kuwa mradi huo utakuwa chachu ya kufungua na kukuza fursa za kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo na mji wa Iringa kwa ujumla.
Akizungumza na Matukio Daima Media kupitia kipindi cha Nyuma ya Kamera, Mbunda alisema licha ya yeye kuwa ni kada wa CHADEMA, hawezi kufumbia macho kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Serikali.
Alisisitiza kuwa maendeleo hayapaswi kuangaliwa kwa misingi ya itikadi za vyama vya siasa bali kwa maslahi mapana ya wananchi wote.
“Maendeleo hayana chama. Barabara hii itawanufaisha wananchi wote wa Mkimbizi bila kujali wanatoka chama gani. ni jukumu letu kama viongozi na wanaharakati wa siasa kupongeza pale kazi nzuri inapofanyika,” alisema Mbunda.
Aidha, Mbunda alimpongeza Diwani wa Kata ya Mkimbizi, Eliud Mvela, kwa juhudi zake za kuendelea kupigania maendeleo ya kata hiyo, hususan ujenzi wa barabara ya lami ambayo kwa muda mrefu imekuwa ni kero kwa wakazi wa eneo hilo, hasa kipindi cha mvua na vumbi wakati wa kiangazi.
Katika hatua nyingine, Mbunda aliipongeza kampuni ya DONETOCLASA REALHOPE (LTD) inayotekeleza mradi huo kwa kazi nzuri na yenye viwango, huku akiitaka kampuni hiyo kutoa kipaumbele cha ajira kwa vibarua wenye sifa kutoka ndani ya Kata ya Mkimbizi ili wananchi wanufaike moja kwa moja na mradi huo.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Jimson Sanga, alisema ujenzi wa barabara hiyo ni muhimu katika kukuza uchumi wa wananchi kwa kuwa utarahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma, kupunguza gharama za usafiri na kuongeza thamani ya maeneo yanayozunguka barabara hiyo.
Sanga aliongeza kuwa miundombinu bora ya barabara ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu, akitoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali na mkandarasi ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.



