KONGANI YA VIWANDA YA GAINI COMPANY LIMITED KUTOA AJIRA 1,500 KWA WANANCHI
Na Matukio Daima Habari
KONGANI ya viwanda ya Gaini Company Limited iliyopo Kata ya Kikongo Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani inatarajiwa uzalisha na kutoa ajira 1,500 ifikapo Machi mwaka huu itakapoanza uzalishaji.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alipotembekea Kongani hiyo ambapo uwekezaji huo unaendana kikamilifu na mkakati wa Serikali wa kukuza uchumi wa viwanda pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, hususani vijana.
Kunenge amesema kuwa Mkoa unaendelea kutekeleza vipaumbele vya Serikali kwa vitendo hususani katika eneo la uzalishaji wa ajira kwa vijana ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.
"Hatua hii inayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Pwani na kuongeza mapato ya Taifa kwa ujumla huku Mkoa ukiendelea kushirikiana na taasisi wezeshi zikiwemo TANESCO, DAWASA na TANROADS ili kuhakikisha hakuna urasimu wowote katika utekelezaji wa masuala ya uwekezaji,"amesema Kunenge.
Amesema kuwa ushirikiano na taasisi hizo ni kuwezesha upatikanaji wa mahitaji muhimu ikiwemo nishati ya umeme, maji pamoja na miundombinu ya barabara na kuwa mradi wa bomba la gesi kutoka Kinyerezi hadi Chalinze tayari umefanyiwa upembuzi yakinifu wa bilioni 2.3 na TPDC jambo litakaloongeza ufanisi wa upatikanaji wa nishati kwa viwanda mkoani humo.
Naye Meneja wa Mradi katika Kongani hiyo QS Bradley Cuthbert Muro amesema kuwa ujenzi wa viwanda viwili umefikia hatua za mwisho ambapo kiwanda cha chuma kimefikia asilimia 85 ya ujenzi huku kiwanda cha cubes kikifikia asilimia 95.
Muro amesema kuwa Kongani hiyo itakuwa na viwanda mbalimbali ikiwemo heavy duty industry, medium industry na light duty industry vikiwemo viwanda vya uzalishaji wa Nondo, Mabati, Steel Pipes, Hallow Sections (RHS) Squqre, Hallow Sections (SHS) Circular, Hallow Sections (CHS) Flat bars pamoja na Misumari.
