MAWAKILI WA MWANDAMBO WATAKA AACHIWE HURU AU AFIKISHWE MAHAKAMANI
Jan 10, 2026
Mawakili Hekima Mwasipu na Philip Mwakilima wamewasilisha maombi ya dharura ya 'Habeas Corpus' katika Mahakama, Masjala Ndogo ya Mbeya, wakitaka Clemence Kenan Mwandambo aachiliwe mara moja au afikishwe mahakamani.
Mwandambo ambaye amekuwa maarufu kupitia Mitandao ya Kijamii na msemo wake wa "Nachoka Mimi mzee wenu Mwandambo", anashikiliwa na Jeshi la Polisi tangu Desemba 29, 2025 bila kufunguliwa mashtaka wala kupewa dhamana.
Nyaraka za Mahakama zilizowasilishwa Januari 9, 2026, Mawakili hao wanahoji kuendelea kushikiliwa kwa Mwandambo ni "kinyume cha Sheria na kunaingilia kwa kiasi kikubwa" haki zake za kikatiba. "Hati ya Dharura" (Certificate of Urgency) iliyoambatana na maombi hayo inabainisha ameshikiliwa kwa muda mrefu zaidi ya Saa 48 uliowekwa Kisheria.
Aidha, Mawakili wanadai kuwa Polisi wamemnyima fursa ya kuonana na Mawakili wake na ndugu zake.
