MBUNGE MWANYIKA AKAGUA MIUNDOMBINU YA BARABARA NJOMBE MJINI
Na Gabriel Kilamlya Matukio Daima Media
NJOMBE
Wananchi wa mtaa wa National Housing Mjini Njombe wameitaka serikali kushughulikia maeneo korofi ya barabara za mtaa huo zilizoharibika kutokana na changamoto ya mvua kwani zinahatirisha usalama wa maisha yao.
Wakazi hao akiwemo Edina Ndenga na Agnes Mtewele wamekiambia kituo hiki kuwa kuharibika kwa miundombinu hiyo ikiwemo mifereji kunawatia hofu hasa kipindi hiki cha mvua ukizingatia maji yamekuwa yakijaa wakati mwingi
Mwenyekiti wa mtaa wa National Housing Malaki Mwandila na Philimon Simba mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM Kata ya Njombe mjini wamesema wakazi wa mtaa huo wamekuwa wakiwatupia lawama juu ya adha hiyo lakini wamekuwa wakikosa majibu.
Mhandisi wa Wakala wa Barabara za mijini na Vijijini TARURA Wilaya ya Njombe Nideo Mwinuka amesema wameanza kushughulikia changamoto hizo na kiasi cha shilingi bilioni 20 zitatukamika kujenga barabara mbalimbali ndani ya kata ya Njombe mjini.
Mbunge wa Jimbo la Njombe mjini Deo Mwanyika amekagua barabara hizo ambazo zimekuwa kikwazo kwa wananchi na kwamba hatua zilizoanza kuchukuliwa na Tarura zitakwenda kuchechemua uchumi wa Wananchi.
Ziara ya mbunge Deo Mwanyika imehusisha ukaguzi wa madaraja,Mitaro pamoja na mabonde hatarishi yaliyoporomoka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.



