MWANDAMBO AACHIWA KWA DHAMANA
Clemence Mwandambo ameachiwa kwa dhamana leo 10 Januari 2026 baada ya kufikishwa kwa siri katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam na kusomewa maombi ya kuwa chini ya uangalizi wa mahakama (Binding Over).
Kwa mujibu wa Wakili wake, Hekima Mwasipu akizungumza na Mwanahalisi TV amesema Mwandambo alifikishwa mahakamani hapo 9 Januari 2026 bila ndugu zake wala mawakili wake kufahamu na kueleza kuwa Mahakama ya Wilaya ya Temeke upande wa Jamhuri uliwasilisha maombi ya Binding Over ukiiomba mahakama itoe amri kadhaa, ikiwemo Mwandambo kutotenda kosa lolote kwa kipindi cha mwaka mmoja, kuripoti katika Kituo cha Polisi Mbeya kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia 9 Januari 2026, pamoja na kutoa akaunti zake zote za mitandao ya kijamii kwa Jeshi la Polisi.
Na mara baada ya kusikiliza maombi hayo, mahakama ilikubaliana na upande wa Jamhuri na kutoa amri hizo na kwa kuwa Mwandambo hakuwa na wakili wala ndugu mahakamani hapo alirejeshwa katika Kituo cha Polisi Chang'ombe baada ya kutoka mahakamani, kabla ya ndugu zake kupigiwa simu siku iliyofuata ambayo ni leo Jumamosi 10 Januari 2026 na kuombwa kumdhamini ambapo mdogo wake Thadeo Mwandambo kumdhamini ndugu yake huyo na kuungana na familia yake iliyopo jijini Dar es Salaam.
Wakili Mwasipu amesema Mwandambo kwa sasa yuko nje kwa dhamana na yupo chini ya uangalizi kwa mujibu wa amri za mahakama, huku akibainisha kuwa Jumatatu ijayo watafanya kikao na mteja wao ili kujadili hatua za kisheria zitakazofuata kwa lengo la kuhakikisha haki zake za msingi zinalindwa.
Itakumbukwa kuwa hapo awali mawakili wa Mwandambo walikuwa wamefungua shauri mahakamani wakidai mteja wao aachiwe kwa dhamana au aachiwe huru, wakisisitiza haki zake za kikatiba na kisheria.
