Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
SERIKALI KUPANUA UTAFITI WA MADINI YA KINYWE KWA USHIRIKIANO NA MAREKANI

SERIKALI KUPANUA UTAFITI WA MADINI YA KINYWE KWA USHIRIKIANO NA MAREKANI

 


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

SERIKALI imetangaza mpango wa kupanua utafiti wa kina wa Madini ya Kinywe kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani, hatua inayolenga kuongeza maarifa ya kitaalamu na kubaini fursa mpya za maendeleo katika sekta ya madini.

Akizungumza jijini Dodoma, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha rasilimali za madini zinatambulika kikamilifu na kutumika kwa manufaa ya Taifa na wananchi.

Mavunde amesema maeneo ya awali yaliyofanyiwa utafiti yanaonesha uwepo wa Madini ya Kinywe katika mikoa ya Lindi na Mtwara, na kwamba Serikali itaendelea kupanua wigo wa utafiti ili kupata takwimu kamili za kijiolojia.

Ameeleza kuwa Watanzania wanaomiliki leseni za uchimbaji wa madini watapewa kipaumbele katika mpango huo, ambapo Serikali itashirikiana na wataalamu wa Marekani kufanya uchambuzi wa kina wa rasilimali hizo.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, jitihada hizo zinatarajiwa kuongeza uzalishaji wa madini hayo kwa siku zijazo, huku makadirio yakionesha kuwa ifikapo mwaka 2050, kiwango kikubwa cha Madini ya Kinywe kitaweza kuzalishwa kila mwaka.


Katika hatua nyingine, Mavunde ameishukuru Serikali ya Marekani kupitia Wizara yake ya Nishati na Madini kwa kuendeleza ushirikiano wa kitaalamu na Tanzania, ikiwemo kusaidia mafunzo ya wataalamu wa ndani.

"Kupitia ushirikiano huo, Watanzania watanufaika na mafunzo ya siku mbili ya kuchambua na kutafsiri takwimu za kijiolojia (Geo Data), yatakayosaidia kuongeza ujuzi katika sekta ya madini, " Amesema Waziri Mavunde. 


Kwa upande wake, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andy Lentz, amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa ushirikiano katika utafiti wa Madini ya Kinywe utakuwa wa muda mrefu.


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3