Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WANANCHI JIJINI MWANZA WAJITOKEZA KUTOA MAONI YA MADHIRA YALIYOTOKEA NOVEMBA 29.

WANANCHI JIJINI MWANZA WAJITOKEZA KUTOA MAONI YA MADHIRA YALIYOTOKEA NOVEMBA 29.

 

NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

Wananchi wa Jijini Mwanza wamejitokeza kwa wingi kutoa taarifa ya madhira kwa Tume ya Uchunguzi wa machafuko yaliyotokea kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana yaliyopelekea vifo, majeraha, na uharibifu wa mali katika maeneo mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari  mjumbe wa Tume hiyo, Balozi Ombeni Sefue ambaye alikuwa Kiongozi wa timu hiyo alisema wamefika kwa ajili ya kuzungumza na wananchi waliopata madhira kwenye tukio hilo na kuwataka waweze kuwa wazi kuzungumza bila uoga wowote kwani wako huru.

Sefue alisema tangia jana walikuwa Jijini hapa wakisikiliza watu waliojitokeza kuelezea madhira waliyokabiliana nayo ambapo kila linalowasilishwa kwao wanachukua kwa ajili kutumiwa katika mchakato wa kuleta maridhiano ya kitaifa ili kujenga mshikamano nchini.

Alisema wamegawanyika katika makundi matatu kutembelea maeneo yaliyokumbwa na adha hiyo ambapo wao wako Mwanza na baada ya hapo watatembelea mikoa ya Geita na Mara.

Alisema wananchi wanawasilisha taarifa zao ana kwa ana, kutumia barua pepe, ujumbe kwa simu, kutuma picha ama taarifa kwenye mawasiliano ya Tume ya Uchunguzi ili kufanyia kazi.

"Watu zaidi ya 100 wamejitokeza kwenye Tume na wanaendelea kuja kutoa taarifa" alisema Sefue.

Mmoja wa shuhuda aliyefika kwenye Tume hiyo, Reuben Gaudence anayeishi Mtaa wa Mecco ambaye duka lake lilichomwa moto ambapo bidhaa ya zaidi ya milioni 68 ziliteketea alisema anapitia kipindi kigumu kwani ameachwa bila kitu.

Aliomba serikali kuangalia namna ya kuwasaidia kukabiliana na changamoto hiyo iliyojitokeza na kumwacha akiwa hana cha kushika kwa sasa.

Deodata Kizanti wa Kisesa wilayani Magu alisema katika machafuko hayo alipoteza mwanaye Leonard James ambaye alikuwa amehitimu kidato cha sita mwaka 2025 kutokana na kupigwa risasi.

Alisema yeye ana miaka 56 na ameshuhudia chaguzi nyingi lakini hakuwahi kuona machafuko ya namna hiyo hivyo aliomba kuwepo kwa mikakati madhubuti kuzuia hali hiyo isijirudie tena hapa nchini.

Meneja wa Luhuye Oil Co Ltd katika eneo la Kisesa alisema gari lao la mafuta lilichomwa pamoja na nyumba ambapo wanakadiria kupata hasara ya zaidi ya milioni 221.7 katika tukio hilo.

Alisema hali hiyo ilifikia hatua hiyo kwa kupuuzwa kwa mahitaji ya uwepo wa Tume huru ya uchaguzi na Katiba Mpya hivyo kuomba kuwepo kwa utashi wa kusikiliza maoni ya wananchi.

 "Tunataka kila mtu anayeathirika na machafuko haya kuweza kutoa taarifa bila hofu yoyote, kwani Tume hiyo ipo kuhakikisha haki inatendeka kwa usawa," alisema Balozi Sefue.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3