Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
DAUD YASSIN: TUZIDI KULIOMBEA  TAIFA ILI VIONGOZI WETU WAENDELEE KUTULETEA MAENDELEO

DAUD YASSIN: TUZIDI KULIOMBEA TAIFA ILI VIONGOZI WETU WAENDELEE KUTULETEA MAENDELEO

  

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Daud Yassin, amewahimiza Watanzania kuendelea kuliombea Taifa ili lidumishe amani na utulivu, akisisitiza kuwa amani ni nguzo muhimu kwa maisha ya binadamu na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Yassin ametoa wito huo leo Jumapili, Januari 18, wakati akishiriki ibada ya Jumapili katika Kanisa la EAG (T) jijini Iringa.

 Akiwahutubia waumini, alisema kuwa amani ni zawadi kubwa kwa Taifa lolote na ni msingi unaowezesha wananchi kuishi kwa uhuru, kufanya kazi zao bila hofu na kushiriki kikamilifu shughuli za kijamii na kidini.

Alieleza kuwa kukosekana kwa amani kuna athari kubwa kwa jamii, kwani husababisha kuvurugika kwa maisha ya kila siku ya wananchi, ikiwemo kushindwa kufanya shughuli za uzalishaji mali, biashara, elimu na hata ibada za kidini.

“Amani ikikosekana, watu watashindwa kufanya shughuli zao za kila siku, ikiwemo kwenda kwenye nyumba za ibada. Maisha yanakuwa magumu na maendeleo husimama,” alisema Yassin.

Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Iringa alisisitiza kuwa jukumu la kuilinda na kuiombea amani si la viongozi pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania bila kujali itikadi za kisiasa au dini. 

Alisema kila mmoja anapaswa kushiriki kwa vitendo na kwa maombi kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa na mshikamano na utulivu.

“Ndugu zangu, ni muhimu sana tuendelee kuiombea nchi yetu bila kuchoka. Amani ni jambo la msingi sana. Hata leo tusingeweza kufika kwenye ibada hii kama kusingekuwa na amani,” aliongeza.

Yassin aliwahimiza pia viongozi wa dini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhimiza maadili mema, upendo, uvumilivu na mshikamano miongoni mwa wananchi, akisema misingi hiyo ndiyo inayojenga Taifa lenye amani ya kudumu.


Wito huo wa Daud Yassin unakuja katika kipindi ambacho viongozi wa dini na Serikali kwa ujumla wamekuwa wakihamasisha wananchi kudumisha mshikamano, kufanya maombi ya pamoja na kulinda amani ya nchi kwa maslahi ya Taifa na vizazi vijavyo, wakitambua kuwa bila amani hakuna maendeleo ya kweli yanayoweza kupatikana.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3