Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
JESHI LA POLISI MKOA WA IRINGA LAWAPATIA NISHANI ZA HESHIMA ASKARI WALIOFANYA VIZURI

JESHI LA POLISI MKOA WA IRINGA LAWAPATIA NISHANI ZA HESHIMA ASKARI WALIOFANYA VIZURI


Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limewapatia nishani za heshima askari wake waliofanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yao kwa mwaka 2025, ikiwa ni sehemu ya kuwatambua na kuwathamini watumishi waliotoa mchango mkubwa katika kulinda amani na usalama wa wananchi.


Akizungumza leo wakati wa hafla fupi ya kuwatunuku nishani hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACAP Allan Bukumbi, amesema kuwa nishani hizo zimetolewa kwa askari wa vyeo vya chini, kufuatia maelekezo ya Jeshi la Polisi nchini yanayolenga kutoa motisha na hamasa kwa askari wanaotekeleza majukumu yao kwa kujituma na uaminifu mkubwa.

Kamanda Bukumbi amesema lengo kuu la utoaji wa nishani hizo ni kuwatia moyo askari waliofanya vizuri zaidi pamoja na kuwahamasisha askari wengine kuongeza juhudi katika kazi zao za kila siku. Amesema utaratibu huo unasaidia kujenga ushindani chanya, kuongeza uwajibikaji na kuimarisha maadili ya kazi ndani ya Jeshi la Polisi.


“Tunatambua mchango mkubwa unaotolewa na askari wetu wa vyeo vya chini ambao wako mstari wa mbele katika kulinda usalama wa raia na mali zao. Kupitia nishani hizi, tunawapa heshima wanayostahili na kuwahamasisha kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uzalendo,” amesema Kamanda Bukumbi.

Hafla hiyo ya utoaji nishani imefanyika katika kilele cha maadhimisho ya Polisi Day, ambayo yalianza rasmi siku ya Jumamosi kwa kutanguliwa na michezo mbalimbali iliyoshirikisha askari wa Jeshi la Polisi na wananchi wa Mkoa wa Iringa. 


Michezo hiyo ililenga kuimarisha mshikamano, ushirikiano na kudumisha mahusiano mema kati ya Jeshi la Polisi na raia, sambamba na kuhimiza jamii kushiriki kikamilifu katika masuala ya ulinzi na usalama.

Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alikuwa mgeni rasmi ambapo amepongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kwa kuendeleza utamaduni wa kuwatambua na kuwazawadia askari wanaofanya vizuri. 

Alisema kuwa zoezi hilo ni muhimu katika kujenga morali ya kazi, kuongeza ufanisi na kuimarisha uwajibikaji miongoni mwa askari.

TAZAMA FULL VIDEO BOFYA LINK HII



















Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3