Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
POLISI WATOA CHETI CHA SHUKRANI KWA MASARI INVESTMENT

POLISI WATOA CHETI CHA SHUKRANI KWA MASARI INVESTMENT


Na Matukio Daima Media 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limetoa cheti cha shukrani kwa Kampuni ya Masari Investment kama kutambua mchango wake katika kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii. 

Cheti hicho kimetolewa leo katika hafla ya Polisi Family Day Iringa 2026 iliyofanyika mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya shughuli maalum za kuimarisha mahusiano, mshikamano na ustawi wa familia za askari polisi pamoja na wadau mbalimbali.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Kheri James, ambaye alikabidhi rasmi cheti hicho kwa niaba ya Jeshi la Polisi. 

Hafla hiyo iliongozwa na mwenyeji wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACAP Allan Bukumbi, aliyetoa pongezi kwa Masari Investment kwa mchango wake unaoonekana katika kusaidia shughuli za kijamii na maendeleo ya ustawi wa askari polisi na jamii kwa ujumla.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, aliipongeza Masari Investment kwa ushirikiano mzuri na Jeshi la Polisi, akisisitiza kuwa ushiriki wa sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kujenga usalama, amani na maendeleo endelevu katika jamii.

 Alitoa wito kwa taasisi na makampuni mengine kuiga mfano huo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Cheti hicho cha shukrani kimepokelewa na Bw. Nasibu Abdula kwa niaba ya Mkurugenzi wa Masari Investment, Bw. Faraj Abri. 

Akipokea cheti hicho, Abdula alieleza shukrani zake kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo, akiahidi kuwa Masari Investment itaendelea kushirikiana na serikali pamoja na vyombo vya ulinzi kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa jamii.

Hafla ya Polisi Family Day Iringa 2026 ilihitimishwa kwa shughuli mbalimbali za kijamii na burudani, zikilenga kuimarisha mshikamano, upendo na ushirikiano miongoni mwa askari polisi, familia zao na wadau.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3