Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MBUNGE KISWAGA ACHAGULIWA KUWA MWENYEKITI KAMATI HII

MBUNGE KISWAGA ACHAGULIWA KUWA MWENYEKITI KAMATI HII

 


Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mheshimiwa Jackson Kiswaga, amechaguliwa rasmi na wajumbe wa kamati ya maji na mazingira ambao ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira.

 Uchaguzi huo umefanyika kwa kuzingatia uzoefu, uwezo na mchango wake katika masuala ya maendeleo, hususan sekta ya maji na uhifadhi wa mazingira, jambo lililowafanya wabunge wengi kumuamini na kumpa jukumu hilo nyeti.

Uchaguzi wa Kiswaga umepokelewa kwa furaha na wananchi wa Jimbo la Kalenga pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo nchini. 

Wananchi Kalenga John kalinga na Zebedaya Sanga wameeleza kuwa nafasi hiyo  ni heshima kubwa kwa jimbo lao na uthibitisho wa imani waliyonayo wabunge juu ya uongozi wa mbunge wao. 

Wamefafanua kuwa nafasi hiyo ni fursa adhimu kwa Kiswaga kuitumia vyema katika kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, ambayo imekuwa kero ya muda mrefu kwa baadhi ya maeneo ya jimbo hilo na sehemu nyingine za nchi.

Wananchi wa Kalenga wameeleza matumaini yao kuwa, kupitia nafasi hiyo, Mbunge wao ataweza kusimamia kwa karibu sera, miradi na bajeti ya sekta ya maji na mazingira ili kuhakikisha kuwa fedha zinazotengwa zinaleta matokeo chanya kwa wananchi. 

Wamesema kuwa changamoto ya uhaba wa maji imeathiri maisha ya kila siku ya wananchi, ikiwemo afya, elimu na shughuli za uzalishaji mali, hivyo wanatarajia kuona kasi mpya katika utekelezaji wa miradi ya maji vijijini na mijini.

Aidha wananchi wamehimiza umuhimu wa kuunganisha juhudi za serikali, sekta binafsi na jamii katika kulinda vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla. 

Wameeleza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila uhifadhi endelevu wa mazingira, misitu na vyanzo vya maji, ambavyo ndivyo uti wa mgongo wa maisha ya binadamu na uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Jackson Kiswaga amewashukuru wabunge kwa imani waliyonayo kwake na kuahidi kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu, uwajibikaji na uzalendo. 

Ameeleza kuwa ataweka mbele maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha kamati inaishauri vyema Serikali ili kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na kulinda mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3