Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
NAIBU MEYA JOHN MREMA ASEMA RAIS SAMIA AMEBADILI TASWIRA YA ELIMU KINYEREZI

NAIBU MEYA JOHN MREMA ASEMA RAIS SAMIA AMEBADILI TASWIRA YA ELIMU KINYEREZI


Na Ashrack Miraji Matukio Daima 

Mkutano rasmi wa wazazi na uongozi wa Shule ya Sekondari  Kinyerezi uliyofanyika tarehe 17 Januari 2026 katika shule hiyo iliyopo Kinyerezi, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujadili masuala ya maendeleo ya elimu na ustawi wa wanafunzi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Diwani wa Kata ya Kinyerezi ambaye pia ni Mhe. Naibu Meya wa Jiji, Mhe. John Lioba Mrema maarufu kwa jina la (Wahenga), pamoja na walimu na wazazi,  ambapo walijadili mafanikio na changamoto zinazoikabili shule hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Naibu Meya John Mrema aliipongeza Shule ya Sekondari Kinyerezi kwa matokeo mazuri ya Kidato cha Pili, akisema kuwa ufaulu huo unaonesha juhudi kubwa za walimu, uongozi wa shule na ushirikiano mzuri wa wazazi.


Aidha, Mhe. Mrema alitumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu kupitia Serikali ya Awamu ya Sita, jambo lililochangia kuboresha miundombinu ya shule na mazingira ya kujifunzia.

Alieleza kuwa kutokana na jitihada za Serikali, Shule ya Sekondari Kinyerezi imepandishwa hadhi na kuanza kufundisha Kidato cha Tano, hatua itakayowarahisishia wanafunzi wa eneo hilo kupata elimu ya juu ya sekondari bila kusafiri umbali mrefu kutafuta shule nyingine.

Mhe. Naibu Meya aliongeza kuwa uongozi wa kata kwa kushirikiana na Halmashauri utaendelea kuunga mkono juhudi zote za kuboresha elimu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miundombinu, walimu na mazingira rafiki ya kujifunzia yanaimarishwa zaidi.

Mkutano huo ulihitimishwa kwa makubaliano ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya wazazi na uongozi wa shule, huku wadau wa elimu wakionesha matumaini kuwa hatua zilizochukuliwa zitachangia kuongeza ufaulu na kuboresha ubora wa elimu katika Shule ya Sekondari Kinyerezi.



 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3