POLISI IRINGA WATOA FARAJA KWA YATIMA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limeendelea kuonesha mshikamano wake na jamii kwa kutembelea na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa vituo viwili vya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu vya Faraja na Dar-Fatma, vilivyopo ndani ya Manispaa ya Iringa, ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watoto.
Akiongoza zoezi hilo la matendo ya huruma Januari 18, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi, amesema kuwa lengo la tukio hilo ni kuendelea kuwa karibu na jamii na kuimarisha ushirikiano katika kulinda haki na ustawi wa watoto.
Miongoni mwa mahitaji yaliyokabidhiwa ni pamoja na sukari, sabuni, mafuta ya kupikia, madaftari, peni pamoja na viroba vya unga.
Aidha, Kamanda Bukumbi ameiasa jamii kuacha vitendo vya ukatili kwa watoto na kuhimiza ushirikiano na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa mapema ili vitendo hivyo viweze kushughulikiwa kwa wakati.
Tukio hilo lilihudhuriwa na askari wa vyeo mbalimbali, ambapo walipata fursa ya kufurahi na watoto hao, wakionesha upendo na mshikamano kwa vitendo.
