RAIS MUSEVENI AVUNJA UKIMYA UVAMIZI WA MAREKANI NCHINI VENEZUELA
Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, ametoa wito kwa mataifa ya Afrika kuimarisha umoja wa kijeshi na kimkakati ili kulinda usalama wa bara hili, akisisitiza kuwa Afrika inaweza kuwa na nguvu kubwa katika vita vya nchi kavu endapo itaungana.
Akizungumza na vijana nchini Uganda tarehe 4 Januari 2026, Rais Museveni amesema kuwa mataifa makubwa kama Marekani yanatawala kwa kiwango kikubwa nyanja za kijeshi zikiwemo anga, bahari na nchi kavu, huku Afrika ikiwa nyuma katika maeneo hayo muhimu ya kiusalama.
Museveni ameonya kuwa udhaifu huo ni tishio kwa usalama wa baadaye wa bara la Afrika, hasa kutokana na kutokuwepo kwa mshikamano wa kijeshi na matumizi ya pamoja ya rasilimali.
Aidha, Rais huyo amewakosoa baadhi ya viongozi wa zamani wa Afrika kwa kushindwa kuhimiza umoja wa kijeshi wa bara, akidai walichagua kubaki kuwa "samaki wakubwa katika kidimbwi kidogo" badala ya kujenga nguvu ya pamoja ya Afrika.
Amesema kukosekana kwa umoja huo kumeifanya Afrika ishindwe kuwekeza kikamilifu katika maendeleo ya kijeshi ya anga na bahari, jambo linaloifanya bara hilo kuendelea kutegemea mataifa ya nje katika masuala ya usalama.
.png)