SERIKALI YAIMARISHA USHIRIKI WA WATANZANIA KATIKA SEKTA YA MADINI
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma.
SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imefanya marekebisho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za mwaka 2018 kwa lengo la kuongeza ushiriki mpana wa Watanzania katika Sekta ya Madini kwa manufaa ya Taifa.
Kupitia marekebisho hayo, Tume ya Madini itaendelea kutangaza mara kwa mara, chini ya Kanuni ya 13A, orodha ya bidhaa na huduma ambazo zinatakiwa kutolewa na kampuni za Kitanzania zinazomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, amesema kuwa Kifungu cha 102 cha Sheria ya Madini kinasisitiza ushiriki wa Watanzania kwa umiliki wa asilimia 100 katika utoaji wa bidhaa na huduma mahsusi migodini.
Waziri Mavunde amesema kuwa katika kipindi cha nyuma kulikuwepo na malalamiko mengi kuhusu wachimbaji na wawekezaji kuagiza karibu bidhaa na huduma zote kutoka nje ya nchi, hali iliyosababisha fedha nyingi za kigeni kutoka nje ya nchi.
Kutokana na changamoto hiyo, Serikali ililazimika kufanya marekebisho ya sheria ili kulinda na kukuza uchumi wa ndani.
Waziri Mavunde ameeleza kuwa, katika miaka ya nyuma, ilikuwa ni nadra kuwakuta Watanzania wakishika nyadhifa za juu katika sekta hiyo, ambapo nafasi nyingi zilishikiliwa na raia wa kigeni.
" Takribani shilingi trilioni 5.1 hutumika kila mwaka katika usambazaji wa bidhaa na huduma migodini kabla ya marekebisho ya sheria, sehemu kubwa ya bidhaa hizo iliagizwa kutoka nje ya nchi, hivyo fedha hizo zilikuwa zikitoka nje kupitia marekebisho hayo, fedha hizo sasa zinatarajiwa kubaki nchini na kuwanufaisha Watanzania moja kwa moja, " Amesema
Amesema Katika kuhakikisha Watanzania wananufaika na fursa za ajira na biashara migodini,Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imekuwa ikihamasisha ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa zinazohitajika kwa wingi katika migodi.
" Kupitia uhamasishaji huo, kampuni mbalimbali zimeanza kuwekeza katika uzalishaji wa bidhaa hizo, zikiwemo Rock Solutions Limited, Max Steel na East Africa Conveyors Supplies Limited, " Amesema.
Aliongeza "Viwanda hivyo vimejengwa kwa ushirikiano na kampuni za kimataifa zinazozalisha bidhaa hizo na kuzisambaza katika nchi mbalimbali duniani, ikiwemo Tanzania, "
Aidha, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imekuwa ikiandaa majukwaa ya kila mwaka yanayowahusisha wamiliki wa leseni za uchimbaji, watoa huduma, wasambazaji wa bidhaa migodini, pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali.
Amesema Lengo la majukwaa hayo ni kutathmini utekelezaji wa kanuni za ushirikishwaji wa Watanzania, kujadili changamoto zilizopo na kuweka maazimio ya kuboresha utekelezaji wake.
"Hadi sasa, Tume ya Madini imeshaendesha majukwaa manne kwa mafanikio makubwa Majukwaa hayo pia huambatana na maonesho ya bidhaa na huduma kutoka kwa kampuni za uchimbaji madini pamoja na watoa huduma migodini, ili kuonesha aina na ubora wa bidhaa na huduma zinazohitajika, " Amesema.
Mwisho




