VIJANA WAITWA MAFUNZO YA KUJITOLEA YA JKT 2026
Jan 20, 2026
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limefungua fursa kwa vijana wa Kitanzania kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kujiunga na mafunzo ya kujitolea yatakayofanyika mwaka 2026.
Akizungumza na wanahabari, Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, amesema kuwa zoezi la uandikishaji na uchukuaji wa vijana litafanyika kupitia mamlaka za serikali za mikoa na wilaya, kulingana na makazi ya waombaji.
Ameeleza kuwa JKT inawapa kipaumbele vijana wenye elimu na ujuzi katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ikiwemo ngazi ya Diploma na Shahada katika fani za TEHAMA, usalama wa mtandao, sayansi ya kompyuta, uhandisi wa kompyuta pamoja na mifumo ya taarifa za biashara.
Aidha, vijana wenye vipaji mbalimbali katika nyanja tofauti pia wanahimizwa kuchangamkia nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mabena, zoezi la usajili litaanza tarehe 26 Januari, likihusisha mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
Vijana watakaofanikiwa kuchaguliwa wanatarajiwa kufika katika makambi ya JKT kuanzia 27 Februari hadi 4 Machi 2026.
"Nisisitize kuwa mafunzo ya JKT hayalengi kutoa ajira za moja kwa moja, wala hayahusiani na ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama au taasisi nyingine za serikali na zisizo za serikali Badala yake, mafunzo hayo yanalenga kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea kiuchumi kupitia stadi za kazi na maisha, " Amesema.
Ameongeza kuwa "Taarifa kamili kuhusu vigezo vya waombaji pamoja na mahitaji muhimu kwa vijana watakaoripoti makambini zinapatikana kupitia tovuti rasmi ya JKT, www.jkt.mil.tz, "
Aidha Brigedia Jenerali Mabena amesema mafunzo ya JKT ni jukwaa muhimu la kuwajenga vijana kimaadili na kimwili, kuimarisha mshikamano wa kitaifa, uzalendo na kuwapa ujuzi utakaowasaidia kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Kwa mujibu wa JKT, waombaji wanapaswa kuwa raia wa Tanzania wenye umri kati ya miaka 16 hadi 18.
Vijana wa Tanzania Bara wanatakiwa kuwa wamehitimu elimu ya darasa la saba, huku kwa Zanzibar wakihitajika kuwa na elimu ya kidato cha pili bila kusahau wahitimu wa kidato cha nne na wahitimu wa elimu ya juu
Waombaji wanapaswa kuwa wamehitimu masomo yao kati ya mwaka 2022 hadi 2025 na kuwa na vyeti halisi vya kuthibitisha elimu hiyo .



