CPA MAKALLA:AMEAHIDI KUSIMAMIA UJENZI WA UKUMBI MKUBWA WA MIKUTANO KILIMANJARO.
Na,Jusline Marco;Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amos Makalla Leo Jan 6,2026 amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo, ambapo aameahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa ujenzi wa Ukumbi mkubwa wa Mikutano wa Kilimanjaro, unaojengwa Mkoani Arusha kwa ubia kati ya kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa umma (PSSSF).
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika ofisini kwake jijini Arusha, CPA Makalla amesema Mkoa wa Arusha ni kitovu cha utalii kwa Kanda ya Kaskazini na ndio mwenyeji wa Mikutano mingi ya Kitaifa na Kimataifa hivyo kujengwa kwa Ukumbi huo kutachochea na kukuza hadhi ya Mkoa katika sekta ya utalii na Mikutano na hivyo kusisimua uchumi wa wananchi wa Arusha.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo akiwa ambatana na Menejimenti ya PSSF amesema ni matumaini yake kuwa ushirikiano wa Wizara na Mkoa wa Arusha utafanikisha ujenzi huo, huku akisema kuwa kukamilika kwa mradi huo wa kimkakati kutaongeza tija kwenye sekta ya utalii, diplomasia na sekta nyingine za kiuchumi, ambapo amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Bw. Fortunatus Magambo kwa ubunifu na ubia wa PSSF na AICC.