DC SAME AWAKA ASIMAMISHA MALIPO YA FUNDI..
SAME.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Same kusitisha mara moja malipo ya fedha ya mwisho kwa fundi aliyetekeleza kazi za mwisho za ujenzi wa bwalo la katika Shule ya Sekondari Kibacha, huku ikiwataka fundi huyo pamoja na fundi wa ufungaji wa madirisha kurejea haraka kwenye mradi huo na kurekebisha kasoro zilizobainika.
Amedai kuwa, mafundi hao wakishindwa kutekeleza agizo hilo ndani ya wiki hii watajifuta kabisa kufanya kazi ndani ya Wilaya ya Same.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni alipofanya ziara ya kushtukiza kukagua utekelezaji wa mradi huo, ikiwa ni ufuatiliaji wa maagizo aliyoyatoa Januari 08, 2026, akiwataka mafundi hao kufanya marekebisho baada ya kubainika kutoridhishwa na ubora wa kazi iliyotekelezwa.
Mkuu wa Wilaya amesema hakuridhishwa na hali ya ukamilishaji wa kazi za ujenzi pamoja na ufungaji wa madirisha, akibainisha kuwepo kwa kasoro zinazokiuka viwango vya ujenzi kwenye hatua za umaliziaji, hali aliyosema inaweza kupunguza thamani ya mradi.