RAIS WA MPITO VENEZUELA AIANGUKIA MAREKANI AOMBA MAZUNGUMZO..
HUKU nchi mbalimbali zikipinga uvamizi wa Marekani Venezuela na kutaka kumwachia huru Rais wa nchi hiyo Rais Nicolas Maduro na mkewe Serikali ya Venezuela imetoa ujumbe kwa jumuiya ya kimataifa na hasa kwa Marekani, ikisisitiza dhamira yake ya kudumisha amani, kuishi kwa kuheshimiana na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa bila vitisho.
Katika taarifa iliyochapishwa katika mitandao ya kijamii leo Jumatatu Januari 5, 2026 na rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez, amesema taifa hilo linaamini kuwa amani ya dunia hujengwa kwa kuhakikisha kwanza amani ndani ya kila nchi.
"Hii ndiyo Venezuela ninayoamini ambayo nimeitolea maisha yangu nina ndoto ya kuona Wavenezuela wote wema wakija pamoja kwa ajili ya taifa lao," amesema.
Rodríguez amesema serikali yake inatoa kipaumbele katika juhudi za kuweka uhusiano wa usawa na wenye kuheshimiana kati ya Venezuela na Marekani, pamoja na mataifa mengine ya ukanda huo, kwa misingi ya usawa wa mamlaka ya mataifa na kutoingiliwa kwa masuala ya ndani.
Aidha, ametoa wito kwa Marekani kufanya mazungumzo ya amani katika ajenda ya maendeleo ya pamoja.
"Tunaialika serikali ya Marekani kushirikiana na sisi katika ajenda ya ushirikiano unaolenga maendeleo ya pamoja ndani ya mfumo wa sheria za kimataifa, ili kuimarisha kuishi kwa amani kwa jamii zetu," amesema Rodriguez.
