WAKANDARASI WAPEWA MAELEKEZO MAKALI MIRADI YA UMEME VITONGOJINI
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amewaelekeza wakandarasi wanaotekeleza miradi ya kusambaza umeme vitongojini kuzingatia nidhamu ya kazi, ubora, maadili na kukamilisha miradi kwa wakati, akisisitiza kuwa serikali haitamvumilia mkandarasi mzembe.
Akizungumza katika hafla ya kusaini mikataba ya shilingi trilioni 1.2 kwa ajili ya kusambaza umeme katika vitongoji 9,009, Waziri Ndejembi amesema upatikanaji wa umeme kwa wote ni ajenda ya kitaifa na ya kimkakati, akibainisha kuwa hakuna uchumi unaoweza kukua bila nishati.
Amesema wakandarasi wanapaswa kutumia lugha nzuri wanapotekeleza miradi kwa wananchi, kujitambulisha kwa viongozi wa ngazi zote ili kuondoa migongano, kushirikisha viongozi wa kisiasa wakiwemo wabunge na madiwani, na kuwasaidia wananchi wasio na uwezo bila kuwabagua.
“Serikali haitavumilia mkandarasi yeyote atakayeshindwa kukamilisha mradi kwa wakati au atakayekiuka masharti ya mkataba hatutaendelea kumpa kazi mkandarasi mzembe,” amesisitiza Waziri Ndejembi.
Ameongeza kuwa wakandarasi wanatakiwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha miradi inadumu na kunufaisha vizazi vijavyo.
Aidha, ametoa maelekezo kuwa shule zote mpya zinazojengwa kwenye majimbo na kata ziunganishwe na umeme, na endapo kutakuwa na jimbo lisilo na huduma hiyo taarifa itolewe mara moja ili hatua zichukuliwe.
Waziri Ndejembi amesema hadi sasa hali ya upatikanaji wa umeme vijijini imefikia asilimia 78, huku serikali ikiwa imekamilisha kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini.
Ameeleza kuwa kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote 64,359 vinatarajiwa kuwa na umeme.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Hassan Said, amesema mradi huo wa shilingi trilioni 1.2 ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi katika sekta ya nishati, ukiwa na lengo la kuunganisha vitongoji 9,009 ndani ya kipindi cha miaka mitatu.
Amesema maandalizi ya mradi yalizingatia vigezo mbalimbali ikiwemo hali ya upatikanaji wa umeme katika vitongoji, na kusisitiza kuwa serikali haitavumilia rushwa wala vitendo vya kuwaonea wananchi, akibainisha kuwa mchango wa mwananchi ni shilingi 27,000 pekee.
Naye Mhandisi Frank Chambua akimwakilisha Mkurugenzi wa shirika la umeme Tanzania TANESCO, amesema REA imekuwa mshirika muhimu katika kusambaza umeme vijijini na elimu itaendelea kutolewa kwa wananchi ili kufuata taratibu sahihi za kuunganishwa na huduma hiyo.
Mwisho
