WANAHARAKATI WALIOSEMA HECHE ANA MPANGO WA KUMUWEKEA LISSU SUMU KUSHTAKIWA..
Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wakili Dkt. Rugemeleza Nshala, Januari 17, 2026, ametoa taarifa kali kufuatia tuhuma zilizotolewa na vijana waliojitambulisha kuwa wanaharakati huru, wakidai kuwa John Heche, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, ana mpango wa kumuwekea sumu kwenye chakula cha Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Tundu Lissu, ambaye yuko gerezani.
Dkt. Nshala amezitaja tuhuma hizo kuwa ni propaganda chafu na za uongo, akisisitiza kuwa hazina msingi wowote wa kisheria wala kimantiki, hasa ikizingatiwa kuwa chakula na vinywaji vya Tundu Lissu vinasimamiwa moja kwa moja na Jeshi la Magereza.
Amesema CHADEMA haitakubali kuona viongozi wake wakichafuliwa hadharani bila kuchukua hatua, hivyo chama kitaanza mara moja kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wanaharakati hao kwa kosa la kuchafua jina, hadhi, heshima na kuaminika kwa John Heche.
“Hawa wote waliomtuhumu John Heche lazima washitakiwe kwa kuchafua jina, hadhi, heshima na kuaminika kwake.
Heche anamuwekeaje Lissu sumu ilhali yuko gerezani na chakula na vinywaji vyake vyote vinatolewa na Jeshi la Magereza? Hizi propaganda chafu lazima zikutane na misuli mikavu ya sheria ili kuzimaliza.
Wamuulize Musiba kuhusu upuuzi huu na nini Mahakama iliamua,” amesema Wakili Dkt. Rugemeleza Nshala.
Kauli hiyo inaongeza msimamo wa CHADEMA wa kupinga vikali tuhuma na taarifa zinazolenga kuchafua viongozi wake, huku ikisisitiza matumizi ya sheria kama njia sahihi ya kulinda heshima na ukweli.
